Baada ya Serikali kutangaza kununua korosho zote mwaka huu na kuwafanya wakulima wakenue kwa furaha, wabanguaji wanakabiliwa na changamoto hivyo kutoa mapendekezo yao.

Wadau wa kilimo nchini wakiwamo wabanguaji wa korosho wameusifu na kuupongeza uamuzi wa kizalendo uliofanyw ana Serikali kuamua kunuua korosho zote kwa bei ya juu ili kumuepushia mkulima hasara.

Hata hivyo, uamuzi huo unawaathiri wabanguaji ambao hawajapata fursa ya kununua malighafi muhimu kwa ajili ya uzalishaji.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema utaratibu unaandaliwa kuhakikisha wadau hawa muhimu wanapata malighafi wanazozihitaji.

“Nitakutana na wadau hivi karibuni kupata maoni yao ni kuona cha kufanya. Wabanguaji ni wazalishaji wa ndani, tunaandaa utaratibu utakaowawezesha kupata malighafi,” anasema Hasunga.

Kiwanda cha Terra

Miongoni mwa wabanguaji nchini ni kiwanda cha Terra Cashew Processing Tanzania Limited kilichopo Kibaha ambacho kilikamilika na kuanza uzalishaji Agosti.

Meneja operesheni wa kiwanda hicho, Gagan Bhurat anasema walianza kufunga mitambo tangu mwanzoni mwa mwaka jana na msimu wa ununuzi ulipofika wakanunua kiasi kidogo kwa ajili ya majaribio.

“Tunaweza kubangua tani 6,000 za ujazo. Kwa sasa hatuna korosho za kutosha isipokuwa chache tulizonunua mwaka jana. Tunasubiri maelekezo ya Serikali kujua utaratibu utakaotuwezesha kununua korosho,” anasema Bhurat.

Kiwanda hicho hubangua korosho kwa ajili ya kuzisafirisha nje ya nchi. Masoko yao ni Marekani, Ulaya na India ambako, anasema korosho za Tanzania zinapendwa sana kutokana na ubora wake.

Ili kuongeza mapato ya Serikali, anapongeza hamasa inayotolewa na Serikali kujenga viwanda vya kubangua zao hilo.

Kuhakikisha uzalishaji wa wabunguaji waliopo unaimaishwa, kiwanda hicho kinapendekeza mambo kadhaa yatakayowasaidia wadau muhimu wa korosho ikiwamo Serikali, wakulima na wabanguaji.

Meneja utawala wa kampuni hiyo, Peter Christopher anasema jambo muhimu ni kuboresha mfumo wa ununuzi wa korosho.

Peter anapendekeza mambo kadhaa kufanikisha hilo. Kwanza ni kuwaruhusu wabunguaji wa ndani kununua kabla ya kampuni za nje ili kuwapa nafasi ya kukusanya mzigo wa kutosha.

Utaratibu huo anasema utawapa fursa ya kununua kwa bei yenye tija kwao pamoja na wakulima pia hivyo kuchochea uchumi wa Taifa kwani wao watapata nafasi ya kuendeleza ubanguaji ambao unahitaji nguvukazi.

Jambo jingine ni ununuzi ufanyike mwaka mzima. Kwa sasa, msimu wa kununua hufanyika kati ya Oktoba na Machi kisha hufungwa.

“Kuna watu huwa wanabakiwa na kiasi kidogo ambazo huziacha mpaka msimu unaofuata. Endapo wanunuzi watakaokuwepo wataruhusiwa kununua wakati wote, itaongeza fursa kwa wabunguaji na wakulima hata Serikali,” anasema Peter.

Kingine kinachoweza kuongeza tija, anasema ni kuwaruhusu wabanguaji kununua moja kwa moja kutoka vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) badala ya kusubiri zipelekwe ghalani.

Hili, anasema litasaidia kupunguza gharama za usafirishaji ambazo huelekezwa kwa mkulima. Lakini, ununuzi huo, anasema bado utaendelea kusimamiwa na vyama vikuu vya ushirika.

Kingine kinachoweza kufanyika, anasema ni kuwapo kwa makubaliano maalumu ya ununuzi wa korosho kati ya vyama vya ushirika na wabanguaji.

“Kila mbanguaji akiwa na vyama vya ushirika vinavyomuuzia korosho, kutakuwa na tija zaidi,” anashauri.

Ubanguaji

Ili kuanza uzalishaji, jumla ya Dola milioni mbili ziliwekezwa na tayari kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 120 wanaobangua tani 330 zilizonunuliwa Machi, 2018.

Meneja operesheni wa kiwanda cha Terra anasema katika kila kilo tano hadi sita za korosho ghafi, hupata kilo moja ya zilizobanguliwa.

Kwa korosho nzuri, anasema kilo tano hutoa moja wakati zile zenye ubora mdogo zinahitajika sita kuipata kilo moja inayofaa kupelekwa sokoni.

Kwa hali ilivyo, anasema: “Tunapata oda kutoka kwa wanunuzi lakini hatuna cha kuwapelekea kwa sababu hatujapata malighafi. Kwa sasa, hata ukiwa na makontena 200 ya korosho, unauza.”

Wasomi

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Omari Mbura anasema kukuza ubanguaji nchini ni lazima viwanda vilivyopo viwe na uhakika wa kupata malighafi.

“Hili linaweza kufanikisha kwa kuwa na utaratibu utakaowaruhusu kununua kutoka kwa Amcos, kumiliki mashamba yao wenyewe au kuingia mkataba na vyama vikuu vya ushirika,” anashauri Dk Mbura.

Mhadhiri mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Dk Fanuel Mlenge anasema mipango ya kina inahitajika kuhakikisha Tanzania inaondokana na usafirishaji wa korosho ghafi.

“Tunalima na kusafirisha. India wanazinunua na kuzibangua, tukianza kufanya kila kitu wenyewe kutakuwa na madhara ndani na nje ya nchi. Umakini unahitajika,” anasema Dk Mlenge.

Categories: Uncategorized

0 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *